< Zaburi 113 >

1 Msifuni Bwana. Enyi watumishi wa Bwana msifuni, lisifuni jina la Bwana. 2 Jina la Bwana na lisifiwe, sasa na hata milele. 3 Kuanzia mawio ya jua hadi machweo yake, jina la Bwana linapaswa kusifiwa. 4 Bwana ametukuka juu ya mataifa yote, utukufu wake juu ya mbingu. 5 Ni nani aliye kama Bwana Mungu wetu, Yeye ambaye ameketi juu kwenye kiti cha enzi, 6 ambaye huinama atazame chini aone mbingu na nchi? 7 Huwainua maskini kutoka mavumbini, na kuwanyanyua wahitaji kutoka kwenye jalala, 8 huwaketisha pamoja na wakuu, pamoja na wakuu wa watu wake. 9 Humjalia mwanamke tasa kutulia nyumbani mwake, akiwa mama watoto mwenye furaha. Msifuni Bwana.

< Zaburi 113 >