< Zaburi 112 >

1 Msifuni Bwana. Heri mtu yule amchaye Bwana, mtu yule apendezwaye sana na amri zake. 2 Watoto wake watakuwa wenye uwezo katika nchi, kizazi cha watu waadilifu kitabarikiwa. 3 Nyumbani mwake kuna mali na utajiri, haki yake hudumu milele. 4 Hata gizani nuru humzukia mtu mwadilifu, yule mwenye rehema, huruma na haki. 5 Mema yatamjia mtu yule aliye mkarimu na mwenye kukopesha bila riba, anayefanya mambo yake kwa haki. 6 Hakika hatatikisika kamwe, mtu mwenye haki atakumbukwa milele. 7 Hataogopa habari mbaya, moyo wake ni thabiti, ukimtegemea Bwana. 8 Moyo wake ni salama, hatakuwa na hofu, mwishoni ataona ushindi dhidi ya adui zake. 9 Ametawanya vipawa vyake kwa ukarimu akawapa maskini; haki yake hudumu milele; pembe yake itatukuzwa kwa heshima. 10 Mtu mwovu ataona na kuchukizwa, atasaga meno yake na kutoweka, kutamani kwa mtu mwovu kutaishia patupu.

< Zaburi 112 >