< Zaburi 101 >

1 Zaburi ya Daudi. Nitaimba juu ya upendo wako na haki yako; kwako wewe, Ee Bwana, nitaimba sifa. 2 Nitazingatia kuishi maisha yasiyo na lawama: utakuja kwangu lini? Nitatembea nyumbani mwangu kwa moyo usio na lawama. 3 Sitaweka mbele ya macho yangu kitu kiovu. Ninayachukia matendo ya watu wasio na imani; hawatashikamana nami. 4 Moyo wa ukaidi utakuwa mbali nami; nitajitenga na kila ubaya. 5 Kila amsingiziaye jirani yake kwa siri, huyo nitamnyamazisha; mwenye macho ya dharau na moyo wa kiburi huyo sitamvumilia. 6 Macho yangu yatawaelekea waaminifu katika nchi, ili waweze kuishi pamoja nami; yeye ambaye moyo wake hauna lawama atanitumikia. 7 Mdanganyifu hatakaa nyumbani mwangu, yeye asemaye kwa uongo hatasimama mbele yangu. 8 Kila asubuhi nitawanyamazisha waovu wote katika nchi; nitamkatilia mbali kila mtenda mabaya kutoka mji wa Bwana.

< Zaburi 101 >