< Mithali 25 >

1 Hizi ni mithali zaidi za Solomoni, zilizonakiliwa na watu wa Hezekia mfalme wa Yuda: 2 Ni Utukufu wa Mungu kuficha jambo, bali ni utukufu wa wafalme kuchunguza jambo. 3 Kama mbingu zilivyo juu na nchi ilivyo chini, ndivyo ambavyo mioyo ya wafalme haichunguziki. 4 Ondoa takataka kwenye madini ya fedha, nako ndani yake kutatokea chombo cha mfua fedha. 5 Ondoa waovu mbele ya mfalme, nacho kiti chake cha enzi kitaimarishwa kwa njia ya haki. 6 Usijikweze mwenyewe mbele ya mfalme, wala usidai nafasi miongoni mwa watu wakuu; 7 ni afadhali yeye akuambie, “Njoo huku juu,” kuliko yeye kukuaibisha mbele ya mkuu. Kile ulichokiona kwa macho yako 8 usiharakishe kukipeleka mahakamani, maana utafanya nini mwishoni kama jirani yako atakuaibisha? 9 Kama ukifanya shauri na jirani yako, usisaliti siri ya mtu mwingine, 10 ama yeye aisikiaye aweza kukuaibisha na kamwe sifa yako mbaya haitaondoka. 11 Neno lisemwalo kwa wakati ufaao ni kama matunda ya mtofaa ya dhahabu yaliyowekwa kwenye vijalizo vya fedha. 12 Kama vile kipuli cha dhahabu au pambo la dhahabu safi, ndivyo lilivyo karipio la mtu mwenye hekima kwa sikio lisikilizalo. 13 Kama vile ubaridi wa theluji wakati wa mavuno ndivyo alivyo mjumbe mwaminifu kwa wale wamtumao, huburudisha roho za bwana zake. 14 Kama vile mawingu na upepo pasipo mvua ndivyo alivyo mtu ajisifuye kwa zawadi ambazo hatoi. 15 Kwa njia ya uvumilivu mtawala aweza kushawishiwa, nao ulimi laini waweza kuvunja mfupa. 16 Ukipata asali, kula kiasi tu cha kukutosha, ukila zaidi, utatapika. 17 Ingiza mguu wako nyumbani kwa jirani yako mara chache, ukizidisha, atakukinai na atakuchukia. 18 Kama vile rungu au upanga au mshale mkali ndivyo alivyo mtu atoaye ushuhuda wa uongo dhidi ya jirani yake. 19 Kama vile jino bovu au mguu uliolemaa, ndivyo ilivyo kumtegemea mtu asiye mwaminifu wakati wa shida. 20 Kama vile avuaye mavazi siku ya baridi, au kama siki iliyomwagwa juu ya magadi, ndivyo alivyo yeye amuimbiaye nyimbo mtu mwenye moyo mzito. 21 Kama adui yako ana njaa, mpe chakula ale; kama ana kiu, mpe maji anywe. 22 Kwa kufanya hivyo, unaweka makaa ya moto yanayowaka kichwani pake, naye Bwana atakupa thawabu. 23 Kama vile upepo wa kaskazini uletavyo mvua, ndivyo ulimi usingiziao uletavyo uso wa hasira. 24 Ni afadhali kuishi pembeni mwa paa la nyumba, kuliko kuishi nyumba moja na mke mgomvi. 25 Kama vile maji baridi kwa nafsi iliyochoka ndivyo zilivyo habari njema kutoka nchi ya mbali. 26 Kama vile chemchemi iliyotibuliwa matope au kisima kilichotiwa taka ndivyo alivyo mtu mwenye haki akishiriki na waovu. 27 Si vyema kula asali nyingi sana, wala si heshima kujitafutia heshima yako mwenyewe. 28 Kama vile mji ambao kuta zake zimebomoka ndivyo alivyo mtu ambaye hawezi kujitawala mwenyewe.

< Mithali 25 >