< Maombolezo 3 >

1 Mimi ndiye mtu aliyeona mateso kwa fimbo ya ghadhabu yake. 2 Amenifukuzia mbali na kunifanya nitembee gizani wala si katika nuru; 3 hakika, amegeuza mkono wake dhidi yangu tena na tena, mchana kutwa. 4 Amefanya ngozi yangu na nyama yangu kuchakaa na ameivunja mifupa yangu. 5 Amenizingira na kunizunguka kwa uchungu na taabu. 6 Amenifanya niishi gizani kama wale waliokufa. 7 Amenizungushia ukuta ili nisiweze kutoroka, amenifunga kwa minyororo mizito. 8 Hata ninapoita au kulia ili kuomba msaada, anakataa kupokea maombi yangu. 9 Ameizuia njia yangu kwa mapande ya mawe, amepotosha njia zangu. 10 Kama dubu aviziaye, kama simba mafichoni, 11 ameniburuta kutoka njia, akanirarua na kuniacha bila msaada. 12 Amevuta upinde wake na kunifanya mimi niwe lengo kwa ajili ya mishale yake. 13 Alinichoma moyo wangu kwa mishale iliyotoka kwenye podo lake. 14 Nimekuwa kichekesho kwa watu wangu wote, wananidhihaki kwa wimbo mchana kutwa. 15 Amenijaza kwa majani machungu na kunishibisha kwa nyongo. 16 Amevunja meno yangu kwa changarawe, amenikanyagia mavumbini. 17 Amani yangu imeondolewa, nimesahau kufanikiwa ni nini. 18 Kwa hiyo nasema, “Fahari yangu imeondoka na yale yote niliyokuwa nimetarajia kutoka kwa Bwana.” 19 Nayakumbuka mateso yangu na kutangatanga kwangu, uchungu na nyongo. 20 Ninayakumbuka vyema, nayo nafsi yangu imezimia ndani yangu. 21 Hata hivyo najikumbusha neno hili na kwa hiyo ninalo tumaini. 22 Kwa sababu ya upendo mkuu wa Bwana, hatuangamii, kwa kuwa huruma zake hazikomi kamwe. 23 Ni mpya kila asubuhi, uaminifu wako ni mkuu. 24 Nimeiambia nafsi yangu, “Bwana ni fungu langu, kwa hiyo nitamngojea.” 25 Bwana ni mwema kwa wale ambao tumaini lao ni kwake, kwa yule ambaye humtafuta; 26 ni vyema kungojea kwa utulivu kwa ajili ya wokovu wa Bwana. 27 Ni vyema mtu kuchukua nira bado angali kijana. 28 Na akae peke yake awe kimya, kwa maana Bwana ameiweka juu yake. 29 Na azike uso wake mavumbini bado panawezekana kuwa na matumaini. 30 Na atoe shavu lake kwa yule ampigaye, na ajazwe na aibu. 31 Kwa kuwa watu hawakatiliwi mbali na Bwana milele. 32 Ingawa huleta huzuni, ataonyesha huruma, kwa kuwa upendo wake usiokoma ni mkuu. 33 Kwa maana hapendi kuwaletea mateso au huzuni watoto wa wanadamu. 34 Kuwaponda chini ya nyayo wafungwa wote katika nchi, 35 Kumnyima mtu haki zake mbele za Aliye Juu Sana, 36 kumnyima mtu haki: Je, Bwana asione mambo kama haya? 37 Nani awezaye kusema nalo likatendeka kama Bwana hajaamuru? 38 Je, si ni kwenye kinywa cha Aliye Juu Sana ndiko yatokako maafa na mambo mema? 39 Mwanadamu yeyote aliye hai aweza kulalamika wakati anapoadhibiwa kwa ajili ya dhambi zake? 40 Tuzichunguze njia zetu na kuzijaribu, na tumrudie Bwana Mungu. 41 Tuinue mioyo yetu pamoja na mikono yetu kwa Mungu mbinguni, na tuseme: 42 “Tumetenda dhambi na kuasi nawe hujasamehe. 43 “Umejifunika mwenyewe kwa hasira na kutufuatilia; umetuchinja bila huruma. 44 Unajifunika mwenyewe kwa wingu, ili pasiwe na ombi litakaloweza kupenya. 45 Umetufanya takataka na uchafu miongoni mwa mataifa. 46 “Adui zetu wote wamefumbua vinywa vyao wazi dhidi yetu. 47 Tumeteseka kwa hofu kuu na shida ya ghafula, uharibifu na maangamizi.” 48 Vijito vya machozi vinatiririka kutoka machoni mwangu, kwa sababu watu wangu wameangamizwa. 49 Macho yangu yatatiririka machozi bila kukoma, bila kupata nafuu, 50 hadi Bwana atazame chini kutoka mbinguni na kuona. 51 Lile ninaloliona huniletea huzuni nafsini kwa sababu ya wanawake wote wa mji wangu. 52 Wale waliokuwa adui zangu bila sababu wameniwinda kama ndege. 53 Walijaribu kukomesha maisha yangu ndani ya shimo na kunitupia mawe; 54 maji yalifunika juu ya kichwa changu, nami nikafikiri nilikuwa karibu kukatiliwa mbali. 55 Nililiitia jina lako, Ee Bwana, kutoka vina vya shimo. 56 Ulisikia ombi langu: “Usikizibie masikio yako kilio changu nikuombapo msaada.” 57 Ulikuja karibu nilipokuita, nawe ukasema, “Usiogope.” 58 Ee Bwana, ulichukua shauri langu, ukaukomboa uhai wangu. 59 Umeona, Ee Bwana, ubaya niliotendewa. Tetea shauri langu! 60 Umeona kina cha kisasi chao, mashauri yao yote mabaya dhidi yangu. 61 Ee Bwana, umesikia matukano yao, mashauri yao yote mabaya dhidi yangu: 62 kile adui zangu wanachonongʼona na kunungʼunikia dhidi yangu mchana kutwa. 63 Watazame! Wakiwa wameketi au wamesimama, wananidhihaki katika nyimbo zao. 64 Uwalipe kile wanachostahili, Ee Bwana, kwa yale ambayo mikono yao imetenda. 65 Weka pazia juu ya mioyo yao, laana yako na iwe juu yao! 66 Wafuatilie katika hasira na uwaangamize kutoka chini ya mbingu za Bwana.

< Maombolezo 3 >