< Yoshua 16 >

1 Mgawanyo wa Yosefu ulianzia Yordani ya Yeriko, mashariki mwa miji ya Yeriko na kutoka hapo ulipanda kupitia jangwani na kuingia katika nchi ya vilima ya Betheli. 2 Ukaendelea kutoka Betheli (ndiyo Luzu), ukavuka kuingia eneo la Waariki huko Atarothi, 3 ukateremkia kuelekea magharibi hadi eneo la Wayafleti ukienea hadi eneo la Beth-Horoni ya Chini hadi Gezeri, ukiishia baharini. 4 Kwa hiyo Manase na Efraimu, wazao wa Yosefu, walipokea urithi wao. 5 Hili ndilo lilikuwa eneo la Efraimu, ukoo kwa ukoo: Mpaka wa urithi wao ulianzia Ataroth-Adari upande wa mashariki hadi Beth-Horoni ya Juu, 6 na kuendelea mpaka baharini. Kutoka Mikmeta upande wa kaskazini ulipinda kuelekea mashariki hadi Taanath-Shilo, ukiupita hadi Yanoa upande wa mashariki. 7 Kisha uliteremka kutoka Yanoa hadi Atarothi na Naara, ukagusa Yeriko na kutokea katika Mto Yordani. 8 Kutoka Tapua mpaka ulikwenda magharibi hadi Bonde la Kana na kuishia baharini. Huu ulikuwa ndio urithi wa kabila la Waefraimu, ukoo kwa ukoo. 9 Pia ulijumuisha miji yote na vijiji vyake ambavyo vilitengwa kwa ajili ya Waefraimu ndani ya urithi wa kabila la Manase. 10 Hawakuwatoa Wakanaani waishio Gezeri; mpaka leo Wakanaani wanaishi miongoni mwa watu wa Efraimu lakini wanatakiwa kufanya kazi ngumu za kulazimishwa.

< Yoshua 16 >