< Yona 2 >

1 Akiwa ndani ya tumbo la nyangumi, Yona alimwomba Bwana Mungu wake. 2 Akasema: “Katika shida yangu nalimwita Bwana, naye akanijibu. Kutoka kina cha kaburi niliomba msaada, nawe ukasikiliza kilio changu. (Sheol h7585) 3 Ulinitupa kwenye kilindi, ndani kabisa ya moyo wa bahari, mikondo ya maji ilinizunguka, mawimbi yako yote na viwimbi vilipita juu yangu. 4 Nikasema, ‘Nimefukuziwa mbali na uso wako, hata hivyo nitatazama tena kuelekea Hekalu lako takatifu.’ 5 Maji yaliyonimeza yalinitisha, kilindi kilinizunguka; mwani ulijisokota kichwani pangu. 6 Nilizama chini sana mpaka pande za mwisho za milima, makomeo ya hiyo nchi yalinifungia hata milele. Lakini uliuleta uhai wangu kutoka shimoni, Ee Bwana Mungu wangu. 7 “Wakati uhai wangu ulipokuwa unatoka, nilikukumbuka wewe, Bwana, nayo maombi yangu yalikufikia wewe, katika Hekalu lako takatifu. 8 “Wale watu wanaongʼangʼana na sanamu zisizofaa hupoteza neema ile ambayo ingekuwa yao. 9 Lakini mimi, kwa wimbo wa shukrani, nitakutolea dhabihu. Lile nililowekea nadhiri nitalitimiza. Wokovu watoka kwa Bwana.” 10 Basi Bwana akamwamuru yule nyangumi, naye akamtapika Yona katika nchi kavu.

< Yona 2 >