< Ayubu 5 >

1 “Ita kama unataka, lakini ni nani atakayekujibu? Ni yupi kati ya hao watakatifu utakayemgeukia? 2 Kuweka uchungu moyoni humuua mpumbavu, nao wivu humchinja mjinga. 3 Mimi mwenyewe nimemwona mpumbavu akistawi, lakini ghafula nyumba yake ikawa imelaaniwa. 4 Watoto wake wako mbali na usalama, hushindwa mahakamani bila mtetezi. 5 Wenye njaa huyala mavuno yake, wakiyatoa hata katikati ya miiba, nao wenye kiu huitamani sana mali yake. 6 Kwa maana taabu haioti kutoka kwenye udongo, wala udhia hauchipui kutoka ardhini. 7 Lakini mwanadamu huzaliwa ili kutaabika, kwa hakika kama cheche za moto zirukavyo kuelekea juu. 8 “Lakini ingekuwa ni mimi, ningemlalamikia Mungu, ningeliweka shauri langu mbele zake. 9 Yeye hutenda maajabu yasiyoweza kutambuliwa, miujiza isiyoweza kuhesabika. 10 Yeye huipa nchi mvua, huyapeleka maji kunyesha mashamba. 11 Huwainua juu wanyonge, nao wale waombolezao huinuliwa wakawa salama. 12 Huipinga mipango ya wenye hila, ili mikono yao isifikie ufanisi. 13 Yeye huwanasa wenye hekima katika hila yao, nayo mipango ya wadanganyifu huifagilia mbali. 14 Giza huwapata wakati wa mchana; wakati wa adhuhuri hupapasa kama vile usiku. 15 Humwokoa mhitaji kutokana na upanga ulioko kinywani mwao; huwaokoa kutokana na makucha ya wenye nguvu. 16 Kwa hiyo maskini analo tarajio, nao udhalimu hufumba kinywa chake. 17 “Heri mtu yule ambaye Mungu humrudi; kwa hiyo usidharau adhabu yake Mwenyezi. 18 Kwa kuwa hutia jeraha, lakini pia huyafunga; huumiza, lakini mikono yake pia huponya. 19 Kutoka majanga sita atakuokoa; naam, hata katika saba hakuna dhara litakalokupata wewe. 20 Wakati wa njaa atakukomboa wewe na kifo, naye katika vita atakukomboa na pigo la upanga. 21 Utalindwa kutokana na kichapo cha ulimi, wala hutakuwa na sababu ya kuogopa maangamizi yatakapokujia. 22 Utayacheka maangamizo na njaa, wala hutakuwa na sababu ya kuwaogopa wanyama wakali wa mwituni. 23 Kwa kuwa utakuwa na agano na mawe ya mashamba, nao wanyama wa mwitu watakuwa na amani nawe. 24 Utajua ya kwamba hema lako li salama; utahesabu mali zako wala hutakuta chochote kilichopungua. 25 Utajua ya kuwa watoto wako watakuwa wengi, nao wazao wako wengi kama majani ya nchi. 26 Utaingia kaburini ukiwa na umri wa uzee mtimilifu, kama masuke ya ngano yakusanywapo kwa wakati wake. 27 “Tumelichunguza hili, nalo ni kweli. Hivyo lisikie na ulitendee kazi.”

< Ayubu 5 >