< Ayubu 17 >

1 Moyo wangu umevunjika, siku zangu zimefupishwa, kaburi linaningojea. 2 Hakika wenye mizaha wamenizunguka; macho yangu yamebaki kutazama uadui wao. 3 “Ee Mungu, nipe dhamana unayodai. Ni nani mwingine atakayeweka dhamana kwa ajili yangu? 4 Umezifunga akili zao zisipate ufahamu, kwa hiyo hutawaacha wapate ushindi. 5 Kama mtu akiwashutumu rafiki zake ili apate ujira, macho ya watoto wake yatashindwa kuona. 6 “Mungu amenifanya kitu cha dhihaka kwa kila mtu, mtu ambaye watu humtemea mate usoni. 7 Macho yangu yamefifia kwa ajili ya majonzi; umbile langu lote ni kama kivuli. 8 Watu wanyofu wanatishwa na hili; watu wasio na hatia wanasimama dhidi ya wasiomcha Mungu. 9 Hata hivyo, waadilifu watazishika njia zao, nao wale wenye mikono safi wataendelea kupata nguvu. 10 “Lakini ninyi njooni, ninyi nyote, jaribuni tena! Sitampata mtu mwenye hekima miongoni mwenu. 11 Siku zangu zimepita, mipango yangu imevunjika, vivyo hivyo shauku za moyo wangu. 12 Watu hawa hufanya usiku kuwa mchana, kwenye giza wao husema, ‘Mwanga u karibu.’ 13 Kama nyumba pekee ninayoitarajia ni kaburi, kama nikikitandika kitanda changu gizani, (Sheol h7585) 14 kama nikiuambia uharibifu, ‘Wewe u baba yangu,’ na kuliambia buu, ‘Wewe u mama yangu’ au ‘Dada yangu,’ 15 liko wapi basi tarajio langu? Ni nani awezaye kuona tarajio lolote kwa ajili yangu? 16 Je, litashuka chini hadi kwenye malango ya mauti? Je, tutashuka pamoja mavumbini?” (Sheol h7585)

< Ayubu 17 >