< Ezekieli 2 >

1 Akaniambia, “Mwanadamu, simama kwa miguu yako nami nitasema nawe.” 2 Alipokuwa akiongea nami, Roho akanijia na kunisimamisha wima, nikamsikia akisema nami. 3 Akaniambia: “Mwanadamu, ninakutuma kwa Waisraeli, kwa taifa asi ambalo limeniasi mimi, wao na baba zao wananikosea mimi hadi leo. 4 Watu ambao ninakutuma kwao ni wapotovu na wakaidi. Waambie, ‘Hivi ndivyo anavyosema Bwana Mwenyezi.’ 5 Kama watasikiliza au hawatasikiliza, kwa kuwa wao ni nyumba ya kuasi, watajua nabii amekuwa miongoni mwao. 6 Nawe mwanadamu, usiwaogope wao wala maneno yao, usiogope, ingawa michongoma na miiba vinakuzunguka na unaishi katikati ya nge. Usiogope yale wasemayo wala usitishwe nao, ingawa wao ni nyumba ya uasi. 7 Wewe lazima uwaambie maneno yangu, ikiwa wanasikiliza au hawasikilizi, kwa kuwa wao ni watu waasi. 8 Lakini wewe mwanadamu, sikiliza ninalokuambia. Usiwe mwenye kuasi kama hiyo nyumba ya kuasi. Fungua kinywa chako na ule nikupacho.” 9 Ndipo nikatazama, nami nikaona mkono ulionyooshwa kunielekea. Nao ulikuwa na ukurasa wa kitabu, 10 ambao aliukunjua mbele yangu. Pande zote mbili ulikuwa umeandikwa maneno ya maombolezo, vilio na ole.

< Ezekieli 2 >