< Kutoka 21 >

1 “Hizi ndizo sheria utakazoweka mbele ya Waisraeli: 2 “Kama ukimnunua mtumwa wa Kiebrania, atakutumikia kwa miaka sita. Lakini katika mwaka wa saba, atakuwa huru naye atakwenda zake pasipo kulipa chochote. 3 Kama akija peke yake, atakwenda huru peke yake, lakini kama akija na mke, ataondoka pamoja naye. 4 Kama bwana wake alimpatia mke naye akamzalia wana au binti, mwanamke pamoja na watoto wake watakuwa mali ya bwana wake na huyo mwanaume ataondoka peke yake. 5 “Lakini kama mtumishi akisema, ‘Ninampenda bwana wangu, mke wangu pamoja na watoto na sitaki kuwa huru,’ 6 ndipo bwana wake atakapolazimika kumpeleka mbele ya waamuzi. Kisha atampeleka kwenye mlango au kizingiti na kutoboa sikio lake kwa shazia. Naye atamtumikia bwana wake maisha yake yote. 7 “Kama mtu akimuuza binti yake kuwa mtumwa, hataachwa huru kama watumwa wa kiume waachiwavyo. 8 Kama hakumpendeza bwana wake aliyemchagua, huyo bwana atamwacha akombolewe. Hatakuwa na haki ya kumuuza kwa wageni, kwa sababu huyo bwana atakuwa amekosa uaminifu. 9 Kama akimchagua aolewe na mwanawe, ni lazima ampe haki za kuwa binti yake. 10 Ikiwa huyo mwana aliyeozwa mtumwa mwanamke ataoa mwanamke mwingine, ni lazima aendelee kumtosheleza huyo mke wa kwanza kwa chakula, mavazi na haki zote za ndoa. 11 Iwapo hatamtosheleza kwa mambo hayo matatu, huyo mke wa kwanza ataondoka na kuwa huru bila malipo yoyote ya fedha. 12 “Yeyote ampigaye mtu na kumuua ni lazima auawe hakika. 13 Hata hivyo, kama hakumuua kwa makusudi, lakini Mungu akaruhusu itendeke, basi atakimbilia mahali nitakapomchagulia. 14 Lakini kama mtu akipanga na kumuua mwingine kwa makusudi, mwondoe katika madhabahu yangu na kumuua. 15 “Yeyote amshambuliaye baba yake au mama yake ni lazima auawe. 16 “Yeyote amtekaye nyara mwingine akamuuza au akamweka kwake, akikamatwa ni lazima auawe. 17 “Yeyote atakayemlaani baba yake au mama yake ni lazima auawe. 18 “Kama watu wakigombana na mmoja akimpiga mwingine kwa jiwe au kwa ngumi yake na hakufa bali akaugua na kulala kitandani, 19 yule aliyempiga ngumi hatahesabiwa kuwa na hatia kama mwenzake ataamka na kujikongoja kwa fimbo yake, lakini hata hivyo, ni lazima amlipe fidia ya muda wake aliopoteza na awajibike mpaka apone kabisa. 20 “Kama mtu akimpiga mtumwa wake wa kiume au wa kike kwa fimbo na mtumwa huyo akafa papo hapo, ni lazima aadhibiwe 21 lakini ikiwa mtumwa ataamka baada ya siku moja au mbili, hataadhibiwa, kwa sababu yule mtumwa ni mali yake. 22 “Ikiwa watu wawili wanapigana na wakamuumiza mwanamke mjamzito, naye akazaa kabla ya wakati lakini hakuna majeraha makubwa, mhalifu atatozwa mali kiasi cha madai ya mume wa yule mwanamke, na jinsi mahakama itakavyoamua. 23 Lakini kukiwa na jeraha kubwa, ni lazima ulipe uhai kwa uhai, 24 jicho kwa jicho, jino kwa jino, mkono kwa mkono, mguu kwa mguu, 25 kuchomwa moto kwa kuchomwa moto, jeraha kwa jeraha, mchubuko kwa mchubuko. 26 “Ikiwa mtu atampiga mtumwa mwanaume au mwanamke kwenye jicho na kuliharibu, ni lazima amwache huru yule mtumwa kama fidia ya hilo jicho. 27 Kama akimvunja jino mtumwa wa kiume au wa kike, ni lazima amwache huru huyo mtumwa kwa kufidia hilo jino. 28 “Kama fahali akimuua mwanaume au mwanamke kwa kumpiga kwa pembe, fahali huyo ni lazima auawe kwa kupigwa mawe, na nyama yake haitaliwa. Lakini mwenye fahali huyo hatawajibika. 29 Lakini hata hivyo, ikiwa huyo fahali amekuwa na tabia ya kupiga kwa pembe, na mwenyewe ameonywa na hakutaka kumfungia naye akamuua mwanaume au mwanamke, huyo fahali ni lazima auawe kwa mawe na mwenye fahali pia auawe. 30 Lakini ikiwa malipo yatatakiwa kwake, basi anaweza kulipa kinachodaiwa ili kuukomboa uhai wake. 31 Sheria hii pia itatumika ikiwa fahali atampiga kwa pembe mwana au binti. 32 Ikiwa fahali atampiga mtumwa wa kike au wa kiume, mwenye fahali atalipa shekeli thelathini za fedha kwa bwana mwenye mtumwa, na fahali ni lazima auawe kwa mawe. 33 “Kama mtu akiacha shimo wazi, ama akachimba shimo kisha asilifukie, na ngʼombe au punda akatumbukia ndani yake, 34 mwenye shimo ni lazima alipe hasara iliyotokea; ni lazima amlipe mwenye mnyama. Mnyama aliyekufa atakuwa wake. 35 “Kama fahali wa mtu fulani atamuumiza fahali wa mtu mwingine na akafa, watamuuza yule aliye hai na wagawane sawa fedha pamoja na mnyama aliyekufa. 36 Hata hivyo, kama ikifahamika kwamba fahali huyo alikuwa na tabia ya kupiga kwa pembe na mwenyewe hakumfunga, ni lazima mwenye fahali alipe mnyama kwa mnyama, na mnyama aliyekufa atakuwa wake.

< Kutoka 21 >