< Mhubiri 4 >

1 Nikatazama tena nikaona uonevu wote uliokuwa unafanyika chini ya jua: Nikaona machozi ya walioonewa, wala hawana wa kuwafariji; uwezo ulikuwa upande wa wale wanaowaonea, wala hawana wa kuwafariji. 2 Nami nikasema kwamba wafu, waliokwisha kufa, wana furaha kuliko watu walio hai, ambao bado wanaishi. 3 Lakini aliye bora kuliko hao wawili ni yule ambaye hajazaliwa bado, ambaye hajaona ule uovu unaofanyika chini ya jua. 4 Tena nikaona kuwa kazi zote na mafanikio yote huchipuka kutokana na wivu wa mtu kwa jirani yake. Hili nalo ni ubatili, ni kukimbiza upepo. 5 Mpumbavu hukunja mikono yake na kujiangamiza mwenyewe. 6 Afadhali konzi moja pamoja na utulivu kuliko konzi mbili pamoja na taabu na kukimbiza upepo. 7 Tena nikaona kitu kingine kilicho ubatili chini ya jua: 8 Kulikuwepo mwanadamu aliye peke yake, hakuwa na mwana wala ndugu. Hapakuwa na mwisho wa kazi yake, hata hivyo macho yake hayakutosheka na utajiri wake. Aliuliza, “Ninajitaabisha hivi kwa ajili ya nani, nami kwa nini ninajinyima kufurahia?” Hili pia ni ubatili, ni shughuli yenye taabu! 9 Wawili ni afadhali kuliko mmoja, kwa sababu wana malipo mazuri kwa kazi yao: 10 Kama mmoja akianguka, mwenzake atamwinua. Lakini ni jambo la kuhuzunisha kwa mtu yule aangukaye naye hana wa kumwinua! 11 Pia, kama wawili wakilala pamoja watapashana joto. Lakini ni vipi mtu aweza kujipasha joto mwenyewe? 12 Ingawa mtu mmoja aweza kushindwa, watu wawili wanaweza kumkabili adui na kumshinda. Kamba ya nyuzi tatu haikatiki kwa urahisi. 13 Afadhali kijana maskini mwenye hekima kuliko mfalme mzee mpumbavu ambaye hajui tena kupokea maonyo. 14 Kijana huyo angeweza kutokea gerezani akapata ufalme, au angeweza kuwa amezaliwa katika umaskini kwenye huo ufalme. 15 Nikaona kwamba wote walioishi na kutembea chini ya jua walimfuata kijana, aliyepokea ufalme. 16 Hapakuwa na kikomo cha watu wote aliowatawala. Lakini wale waliokuja baadaye hawakufurahia kazi ya yule aliyepokea ufalme. Hili nalo pia ni ubatili, ni kukimbiza upepo.

< Mhubiri 4 >