< 1 Samweli 2 >

1 Kisha Hana akaomba na kusema: “Moyo wangu wamshangilia Bwana, katika Bwana pembe yangu imeinuliwa juu. Kinywa changu chajisifu juu ya adui zangu, kwa kuwa naufurahia wokovu wako.
Hana aliomba akasema, “moyo wangu wamtukuza BWANA. Pembe yangu imejulikana katika BWANA. Kinywa changu kinatamba dhidi ya maadui zangu, kwa kuwa naufurahia wokovu wako.
2 “Hakuna yeyote aliye mtakatifu kama Bwana, hakuna mwingine zaidi yako; hakuna Mwamba kama Mungu wetu.
Hakuna aliye mtakatifu kama BWANA, kwa kuwa hakuna mwingine zaidi yako; hakuna mwamba kama Mungu wetu.
3 “Msiendelee kusema kwa kiburi hivyo wala msiache vinywa vyenu kunena kwa kiburi, kwa kuwa Bwana ndiye Mungu ajuaye, na kwa yeye matendo hupimwa.
Msijivune sana hivyo kwa kiburi; vinywa vyenu visitoke majivuno. Kwa kuwa BWANA ni Mungu wa maarifa; yeye huyapima matendo kwa mizani.
4 “Pinde za mashujaa zimevunjika, lakini wale wanaojikwaa wamevikwa nguvu.
Pinde za mashujaa zimevunjika, bali wale wanaojikwaa hujivika nguvu kama mshipi.
5 Wale waliokuwa na chakula tele wamejikodisha wenyewe ili kupata chakula, lakini wale waliokuwa na njaa hawana njaa tena. Mwanamke yule aliyekuwa tasa amezaa watoto saba, lakini yule ambaye alikuwa na wana wengi amedhoofika.
Wale walio na shibe ya kutosha wamejikodisha ili wapate chakula; wale waliokuwa na njaa hawana njaa tena. Hata yule aliye kuwa tasa amezaa watoto saba, bali mwanamke mwenye watoto wengi amenyong'onyea.
6 “Bwana huua na huleta uhai, hushusha chini mpaka kaburini na hufufua. (Sheol h7585)
BWANA huua na huuisha. Hushusha kuzimu na huleta tena juu. (Sheol h7585)
7 Bwana humfanya mtu maskini naye hutajirisha, hushusha na hukweza.
BWANA humfanya maskini, na yeye ndiye humtajirisha mtu. Yeye hudhili, lakini pia hukweza
8 Humwinua maskini kutoka mavumbini na humwinua mhitaji kutoka lundo la majivu; huwaketisha pamoja na wakuu na kuwafanya warithi kiti cha enzi cha heshima. “Kwa kuwa misingi ya dunia ni ya Bwana; juu yake ameuweka ulimwengu.
Yeye humwinua juu maskini toka mavumbini: Huwainua wahitaji toka jalalani na kuwaketisha pamoja na wakuu na kuwarithisha kiti cha enzi cha utukufu. Kwa kuwa nguzo za dunia ni za BWANA na ameukalisha ulimwengu juu yake.
9 Yeye atailinda miguu ya watakatifu wake, lakini waovu watanyamazishwa kwenye giza. “Si kwa nguvu mtu hushinda;
Yeye atazilinda nyayo za watu wake waaminifu, bali waovu watanyamazishwa gizani, kwa maana hakuna atayeshinda kwa nguvu zake.
10 wale wampingao Bwana wataharibiwa kabisa. Atapiga radi dhidi yao kutoka mbinguni; Bwana ataihukumu miisho ya dunia. “Atampa nguvu mfalme wake, na kuitukuza pembe ya mpakwa mafuta wake.”
Wale wampingao BWANA watavunjwa vipande vipande; atawapiga radi kutokea mbinguni. BWANA atahukumu miisho ya dunia; atampa nguvu mfalme wake na kuinua pembe ya mtiwa mafuta wake.”
11 Kisha Elikana akaenda nyumbani Rama, lakini mtoto akahudumu mbele za Bwana chini ya kuhani Eli.
Nndipo Elikana akenda Rama, nyumbani kwake. Na yule mtoto akamtumikia BWANA machoni pa Eli, kuhani.
12 Wana wa Eli walikuwa watu wabaya kabisa, hawakumheshimu Bwana.
Basi, watoto wa Eli walikuwa wakorofi. Wao hawakumheshimu BWANA.
13 Basi ilikuwa desturi ya makuhani pamoja na watu kwamba kila mara yeyote anapotoa dhabihu na huku nyama ikiwa inachemshwa, mtumishi wa kuhani angalikuja na uma wenye meno matatu mkononi mwake.
Desturi ya makuhani na watu ilikuwa kwamba endapo mtu yeyote ametoa dhabihu, mtumishi wa kuhani angekuja akiwa na uma wa meno matatu mkononi mwake, nyama ilipokuwa inatokoswa.
14 Angeutumbukiza huo uma kwenye sufuria au birika au sufuria kubwa au chungu, naye kuhani angalijichukulia mwenyewe chochote ambacho uma ungekileta. Hivi ndivyo walivyowatendea Waisraeli wote waliokuja Shilo.
Naye angeutia uma huo sufuriani, au birikani au chomboni au chunguni; nyama yote ambayo ingeinuliwa na uma huo ingetwaliwa na kuhani mwenyewe. Ndivyo walivyofanya huko Shilo kwa Waisraeli wote waliokwenda huko.
15 Lakini hata kabla mafuta ya mnyama hayajachomwa, mtumishi wa kuhani angalikuja na kusema kwa mtu ambaye alikuwa akitoa dhabihu, “Mpe kuhani nyama akaoke, kwani hatapokea nyama iliyochemshwa kutoka kwako, ila iliyo mbichi tu.”
Tena, kabla ya kuteketeza mafuta, mtumishi wa kuhani alikuja, na kumwambia aliyekuwa akitoa dhabihu, “Tenga nyama ya kuchoma kwa ajili ya kuhani; kwa sababu hataikubali ile ya kutokosa kutoka kwako, bali tu ile mbichi.”
16 Kama mtu akimwambia, “Mafuta ya mnyama na yachomwe kwanza, ndipo uchukue chochote unachotaka,” mtumishi angalijibu, “Hapana, nipe sasa, kama huwezi nitaichukua kwa nguvu.”
Ikiwa mtu atamwambia, “Wachome mafuta kwanza, na kisha uchukue kiasi utakacho.” Ndipo angesema, “Hapana, utanipatia sasa hivi; la sivyo; Nitaichukua kwa lazima.”
17 Hii Dhambi ya hawa vijana ilikuwa kubwa sana machoni pa Bwana, kwa kuwa waliitendea dhabihu ya Bwana kwa dharau.
Dhambi ya vijana hawa ilikuwa mbaya sana mbele za BWANA, kwa sababu waliidharau dhabihu ya BWANA.
18 Lakini Samweli alikuwa akihudumu mbele za Bwana, kijana akivaa kisibau cha kitani.
Lakini Samweli alimtumikia BWANA akiwa mdogo akivaa nguo ya naivera ya kitani.
19 Kila mwaka mama yake alimshonea joho dogo na kumchukulia wakati alipokwea pamoja na mumewe kutoa dhabihu ya mwaka.
Kila mwaka mama yake alimtengenezea kanzu dogo na kumletea, wakati wakija na mmewe kutoa dhabihu ya kila mwaka.
20 Eli alikuwa akiwabariki Elikana na mkewe, akisema, “Bwana na akupe watoto kwa mwanamke huyu ili kuchukua nafasi ya yule aliyekuwa amemwomba na akamtoa kwa Bwana.” Kisha wakawa wanakwenda nyumbani.
Eli aliwabariki Elikana na mke wake na kusema, “BWANA akupatie watoto zaidi kwa mwanamke huyu kwa sababu ya ahadi yake aliyoitoa kwa BWANA.” Baadaye walirudi nyumbani kwao.
21 Bwana akawa mwenye neema kwa Hana, naye akapata mimba akazaa wana watatu na binti wawili. Wakati huo, kijana Samweli akaendelea kukua mbele za Bwana.
BWANA alimsaidia tena Hana, akawa amebeba mimba nyingine. Akazaa watoto watatu wa kiume na wa kike wawili. Wakati huo huo mtoto Samweli akakua akiwa mbele za BWANA.
22 Basi Eli, ambaye alikuwa mzee sana, alisikia kuhusu kila kitu ambacho wanawe walikuwa wakiwafanyia Israeli wote na jinsi walivyokutana kimwili na wanawake waliohudumu kwenye ingilio la Hema la Kukutania.
Basi Eli alikuwa mzee sana, akayasikia yote ambayo watoto wake walikuwa wakiwafanyia Waisraeli wote, na jinsi walivyotembea na mwanamke aliyekuwa akitumika katika lango la hema ya kukutania.
23 Hivyo akawaambia, “Kwa nini mmefanya mambo kama haya? Nimesikia kutoka kwa watu wote juu ya haya matendo yenu maovu.
Akawaambia, “Kwa nini mnafanya mambo hayo? Kwa maana nasikia matendo yenu maovu kutoka kwa watu hawa wote.”
24 Sivyo, wanangu, hii si habari nzuri ambayo ninasikia ikienea miongoni mwa watu wa Bwana.
Sivyo hivyo, watoto wangu, maana hii ninayoisikia siyo taarifa njema. Mnawakosesha watu wa BWANA.
25 Kama mtu akifanya dhambi dhidi ya mtu mwenzake, mtu mwingine aweza kumwombea kwa Mungu, lakini kama mtu akimfanyia Mungu dhambi, ni nani atakayemwombea?” Hata hivyo wanawe hawakusikia maonyo ya baba yao, kwa sababu Bwana alitaka kuwaua.
“Kama mtu mmoja akimkosea mwenzake, Mungu atamhukumu; Lakini mtu akimkosea BWANA, ni nani atakayemtetea mtu huyo?” Lakini hawakuitii sauti ya baba yao, sababu BWANA alinuia kuwaua.
26 Naye kijana Samweli akaendelea kukua katika kimo, akimpendeza Bwana na wanadamu.
Yule mtoto Samweli aliongezeka umri, na kupata kibali kwa BWANA na kwa watu pia.
27 Basi mtu wa Mungu akaja kwa Eli na kumwambia, “Hivi ndivyo asemavyo Bwana: ‘Je, sikujifunua waziwazi kwa nyumba ya baba yako wakati walikuwa huko Misri chini ya Farao?
Kisha mtu wa Mungu akamwendea Eli na kumwambia, “BWANA asema, 'Je, sikujifunua mwenyewe kwa nyumba ya baba zako, walipokuwa Misri utumwani nyumbani mwa Farao?
28 Nilimchagua baba yako kati ya makabila yote ya Israeli kuwa kuhani wangu, kukwea kwenye madhabahu yangu, kufukiza uvumba na kuvaa kisibau mbele yangu. Pia niliwapa nyumba ya baba yako sadaka zote zilizotolewa kwa moto na Waisraeli.
Mimi nilimchagua yeye kutoka makabila yote ya Israeli awe kuhani wangu, apande madhabahuni kwangu, na kufukiza uvumba, na kuvaa kanzu ya naivera mbele yangu. Niliwapa nyumba ya baba zako dhabihu zote za wana wa Israeli zilizotolewa kwa moto.
29 Kwa nini unadharau dhabihu zangu na sadaka zile nilizoziamuru kwa ajili ya makao yangu? Kwa nini unawaheshimu wanao kuliko mimi kwa kujinenepesha wenyewe kwa kula sehemu zilizo bora za kila sadaka zinazotolewa na watu wangu wa Israeli?’
Kwanini basi, unaidharau dhabihu yangu na sadaka ambazo ninazitaka mahali ninapoishi? Kwanini unawaheshimu watoto wako kuliko mimi, kwa kujinenepesha ninyi wenyewe kwa uzuri wa kila sadaka ya watu wangu Israeli?'
30 “Kwa hiyo, Bwana, Mungu wa Israeli asema: ‘Niliahidi kuwa nyumba yako na nyumba ya baba yako wangehudumu mbele zangu milele.’ Lakini sasa Bwana anasema: ‘Jambo hili na liwe mbali nami! Wale wanaoniheshimu nitawaheshimu, wale wanaonidharau mimi watadharauliwa.
Maana, BWANA, Mungu wa Isareli, asema, niliahidi kwamba nyumba yako, na nyumba ya baba yako, yawapasa kwenda mbele zangu milele,' Lakini sasa BWANA asema. 'Mambo haya yapishe mbali. nami nisifanye hivi, maana nitawaheshimu wanaoniheshimu, bali wanaonidharau mimi hawatakuwa na thamani.
31 Wakati unakuja nitakapozipunguza nguvu zenu na nguvu ya nyumba ya baba yenu, ili pasiwepo mtu katika mbari yenu atakayeishi kuuona uzee
Tazama, siku zinakuja nitakapoondoa nguvu zako na nguvu za nyumba za baba yako, ili kwamba pasije kuwepo mtu mzee katika nyumba yako.
32 nanyi mtaona huzuni katika makao yangu. Ingawa Israeli watafanyiwa mema, katika mbari yenu kamwe hapatakuwepo mtu atakayeishi hadi kuwa mzee.
Nawe utalitazama hangaiko katika makao yangu. Ingawa Israeli watapewa jambo jema, hapatakuwapo tena mtu yeyote mzee katika nyumba yako.
33 Kila mmoja wenu ambaye sitamkatilia mbali kutoka madhabahuni pangu atabakizwa tu kupofusha macho yenu kwa machozi na kuihuzunisha mioyo yenu, nao wazao wenu wote watakufa watakapokuwa wamefikia umri wa kustawi.
Yeyote miongoni mwenu nisiye mwondoa kutoka madhabahuni pangu, Nitasababisha macho yenu yaanguke, na ita nitasababisha huzuni maishani mwenu. Wanaume wote waliozaliwa katika familia yako watakufa.
34 “‘Kile kitakachotokea kwa wanao wawili, Hofni na Finehasi, kitakuwa ishara kwako. Wote wawili watakufa katika siku moja.
Hii ndiyo itakuwa ishara kwako ambayo itawaijia watoto wako wakiume wawili, juu ya Hofni na Finehasi: Wote wawili watakufa siku moja.
35 Mimi mwenyewe nitajiinulia kuhani mwaminifu, ambaye atafanya sawasawa na kile kilichoko moyoni mwangu na akilini mwangu. Nitaifanya nyumba yake kuwa imara, naye atahudumu mbele ya mpakwa mafuta wangu daima.
Nami nitamwinua juu kuhani wangu mwaminifu atakaye fanya kile kilichomo moyoni mwangu na nafisini mwangu. Nami nitamjengea nyumba madhubuti; naye atakwenda mbele ya mfalme wangu mbarikiwa milele.
36 Kisha kila mmoja aliyeachwa katika mbari yenu atakuja na kusujudu mbele yake kwa ajili ya kipande cha fedha na ganda la mkate akisema, “Niteue katika baadhi ya ofisi ya ukuhani ili niweze kupata chakula.”’”
Kila mmoja aliyebakia nyumbani mwako atakuja na kusujudu mbele ya mtu huyo, akiomba kipande cha fedha na mkate mmoja, naye atasema, “Tafadhali uniajiri katika moja ya nafasi za kuhani ili niweze kula kipande cha mkate'”'

< 1 Samweli 2 >